Msaga Sumu: Sikunufaika na Wimbo Wangu wa Kampeni Niliomwimbia Edward Lowassa....Wanaosema Nilijengewa Nyumba Waongo - MULO ENTERTAINER

Latest

15 Mar 2016

Msaga Sumu: Sikunufaika na Wimbo Wangu wa Kampeni Niliomwimbia Edward Lowassa....Wanaosema Nilijengewa Nyumba Waongo

MSANII wa nyimbo za Uswahilini ‘Kigodoro’, Seleman Jabir ‘Msaga Sumu’, ameweka wazi kwamba licha ya kupata jina kubwa katika kampeni za urais na wabunge mwaka 2015, lakini hakunufaika na wimbo aliowatungia wagombea hao.

msaga sumu
Msaga Sumu aliweka wazi hayo jana alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Bingwa, Dimba na The African zilizopo Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo alilalama kwamba licha ya kutunga wimbo uliomtaja aliyekuwa mgombea urais wa Chadema kupitia mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa, lakini hakunufaika nao kama watu wanavyodhani.

“Wimbo haukuninufaisha chochote kama baadhi ya watu wanavyosema kwamba nimejengewa nyumba na nimenunuliwa gari, nilichopata ni fedha ya mboga na kufahamu baadhi ya mikoa ya Tanzania ambayo sikuwa
nikiifahamu ukiwemo Mwanza, Mbeya, Tabora na mingineyo.

“Nilipoona hakuna maslahi nikamweleza Mzee Lowassa tulipokutana naye mkoani Morogoro katika kikao cha pamoja na wasanii wengine, hapo nilimweleza dukuduku langu hilo na ndipo tukakubaliana upya kwa mikoa mitano nikalipwa kwa mikoa hiyo tu.

“Kwanza watu wajue kwamba wimbo wa Lowassa niliuimba kipindi alipokuwa CCM, lakini sikutaja chama
chochote ila alipohamia Chadema alihama nao wakaniita nikatie maneno ya Chadema,” alieleza Msaga Sumu.

Katika hatua nyingine mkali huyo wa ‘Kigodoro’ alisema yupo mbioni kuachia wimbo wa timu anayoipenda kwa Tanzania, Yanga Africans ili kulipa fadhili ya wimbo aliowaimbia mashabiki wa Simba.
“Mimi ni mwana Yanga lakini niliimba wimbo wa Simba kwa kuwa Simba walikuwa bora kwa kipindi kile lakini kwa sasa nimeandaa wimbo mpya wa Yanga ambao utakuwa mkali kuliko ule wa Simba, naomba mashabiki wangu wakae mkao wa kusubiri kwa hamu wimbo huo,’’ alieleza.

Mtanzania