Nawasalimu wa jina la YESU, jina kuu kupita majina yote. Jina langu ninaitwa Theoflida , ni mwanamke mwenye umri wa miaka 38 mkaazi wa Mbezi ya Kimara jijini Dar Es Salaam, japo kiasili ni mwenyeji wa wilaya ya Ulanga, mkoani Morogoro..
Nime amua kuandika waraka huu kwa madhumuni makuu mawili, kwanza ni kushuhudia MATENDO MAKUU ambayo YESU AMENITENDEA na pili, ni kuwa hasa wanawake wenzangu kutojihusisha kabisa na masuala ya WAGANGA WA KIENYEJI kwa sababu waganga wa kienyeji ni MAWAKALA WA KAZI ZA SHETANI HAPA DUNIANI na ni MASHETANI KABISA!...
Nitaanza kwa kuelezea kisa kilicho nipelekea kuingia kichwa kichwa kwenye mikono ya wakala wa shetani..
Nilikuwa nimepanga chumba kimoja maeneo ya Tabata Mawenzi huku nikijihusisha na biashara ya genge. Jirani na nyumba niliyokuwa nimepanga, aliishi mwanaume mmoja na mke wake. Mwanaume huyu jina lake linaanzia na herufi K hivyo katika maelezo yangu nitakuwa nikimtaja kwa herufi K.
K alikuwa ni mwanaume mwenye mafanikio makubwa katika maisha mwenye kazi nzuri. Alikuwa na nyumba zaidi ya moja, magari ya kifahari. viwanja , mashamba, na miradi mbalimbali iliyokuwa ikimlipa vizuri sana. Kwa ufupi K alikuwa tajiri mwenye maisha mazuri.
K na mke wake wote walikuwa wenyeji wa wilaya ya Muleba,mkoani Kagera . Ndoa ya K na mkewe ilikuwa na umri wa mwaka mmoja...
K na mke wake waliishi maisha mazuri sana....Kwa sababu ya ugumu wa maisha yangu, nikajikuta naanza kutamani maisha ya mke wa K.. Nikawa natamani mimi ndo ningekuwa mke wa K na kufurahia maisha vile mke wa K alivyo kuwa akifurahia. Nilimuona mke wa K kama mtu mwenye bahati sana na kutamani bahati hiyo iwe yangu.
Baada ya wazo hili kukomaa ndani ya nafsi yangu, nikaanza kutafuta njia ya kumteka K kimapenzi na kuchukua nafasi ya mke wake. Njia pekee niliyo ona inafaa, ni kutumia uchawi.
Sasa basi, kuna rafiki yangu mmoja, anaitwa Pamela. Pamela alikuwa anapenda sana mambo ya waganga waganga, kwa hivyo alikuwa anawajua waganga wengi. Hata katika biashara yangu ya genge, alishanipeleka kwa waganga kadhaa kwa ajili ya kupata dawa ya mvuto wa bishara yangu..
Nilipo mfuata Pamela, akaniambia kuna mganga mmoja, ni mkali sana wa mambo ya mapenzi.. Mi mwenyewe nina mpango wa kumtafuta lakini najipanga kwanza kwa sababu bei zake ni kubwa.
Pamela akasema alimfahamu mganga huyo alipokuwa katika kijiji cha Mwalusembe, wilayani Mkuranga.. Siku hiyo kuna fumanizi lilitokea, mwanaume alikuwa anatembea na mke wa mtu, kumbe huyo mwanamke alikuwa amewekewa tego, huyo mwanaume alipo muingilia mwanamke huyo, wakawa wamenasana.. Baadae ikatafutwa namba ya simu ya mume wa mwanamke. Mume alipofika kufumania, akakuta mke wake amenasana na mgoni wake.. Akaitwa huyo Mganga kwa sababu ndie aliye weka hilo tego, alipofika eneo la tukio alifanya uganga wake, wale wagoni wakawa wameachana.. Tukio hilo lilivuta watu wengi sana.. Kwa hiyo Pamela anasema, alimjulia mganga huyu kwenye tukio hilo... Akafanikiwa kutafuta na kupata namba zake.
Pamela akanipa namba za simu za mganga huyo, nilivyo mpiugia akasema yupo Handeni kikazi ila baada ya siku tatu atakuwa Bagamoyo ambapo atakaa hapo kwa mwezi mzima aki agua watu wenye matatizo mbalimbali.
Kweli baada ya siku ya tatu, nikaenda hadi Bagamoyo kuonana na huyo mganga ambaye jina lake tu ni kufuru kubwa kwa Mungu.,. Yeye anajiita MUNGU WA KABILI ambayo tafsiri yake ni MUNGU WA PILI. Lakini pia nilishangaa kumuona mganga mwenyewe anaokena bado kijana ambaye sidhani kama ana fikisha miaka arobaini.
NAANZA KWA KUPIMWA MWILI WANGU KICHAWI
Mungu wa Kabili akasema kabla, hajaanza kazi ya ‘kumtengeneza’ K , inabidi aanze kwanza kuuangalia mwili wangu ili ajue kama ni msafi ama mchafu.
Basi nikapewa dawa nimeze, halafu nikaambiwa Yule kuku mweusi ambaye nilienda nae mwenyewe, nimshike kichwani. Baada ya hapo, Dokta Mungu wa Kabili akaanza kuongea maneno yake ya kiganga huku akiwa ameshikilia chungu chenye dawa iliyo katika mfumo wa maji maji.. Alifanya hivyo kwa muda wa kama dakika kumi na tano hivi. Alipomaliza kufanya uganga wake, akaniambia nimtue Yule kuku mweusi niliekuwa nimembeba kichwani. Nilipo mtua nikashangaa kumuona kuku Yule amekufa. Niliogopa sana .
Basi Mungu wa Kabili, akaniambia mwili wangu ni mchafu sana. Roho ya mauti imepandwa kwenye mwili wangu. Hivyo lazima anisafishe kwanza, kutoa uchafu ulio pandikizwa mwilini wangu kichawi. Baada ya hapo ndio tutaendelea na zoezi la kumfanyia ulozi K.
Mungu wa Kabili akaniambia niende nyumbani, nirudi siku inayo fuata jioni ya saa kumi na mbili nikiwa na sarafu 350 za shilingi mia mbili mbili ambazo jumla yake ni Shilingi Elfu Sabini, mchanga wa njia panda saba, pamoja na wembe tatu..
NASAFISHWA MWILI WANGU KICHAWI.
Ilipo fika saa sita kamili za usiku, mimi , Dokta Mungu Wa Kabili pamoja na msaidizi wake, tukaongozona hadi njia panda. Njia panda hiyo ipo huko huko Bagamoyo porini..
Tulibeba, kigoda, chungu , vifaa nilivyo kuja navyo ( mchanga, wa njia panda saba, sarafu 350, pamoja na asali nusu lita ), mawe matatu, mishumaa ya rangi nyekundu, mkaa, pamoja na dawa nyingine zilizokuwa kwenye vibuyu kama saba hivi.
Tulipofika eneo la njia panda, Mungu wa Kabili, alizungushia dawa kuzunguka eneo tulipoweka vitu vyetu, akamuagiza msaidizi wake, awashe mishumaa ambayo idadi yake ilikuwa kumi na nne, mishumaa hiyo iliwekwa kuzunguka eneo tulilokuwa sisi. Baada ya hapo, ukawasha moto, kwenye mafiga kisha chungu kikatengwa pale, nikaweka vitu vyangu vyote nilivyo kuja navyo, na yeye Mungu wa Kabili, akachanganya dawa zake anazo zijua mwenyewe…
Baada ya kama dakika arobaini hivi, zile dawa zikawa zimecheka, nikapewa kibuyu nikaambiwa nikoge kwa kuchota maji ya kwenye chungu huku chungu kikiwa kinachemka. Nikafanya kama nilivyo elekezwa huku mganga akiwa anaongea vitu vyake vya kiganga ambavyo sikuweza kuvielewa..
Nilipomaliza kuoga, mganga akanichanja karibu mwili mzima, kisha nikapakwa hiyo asali. Baada ya hapo, tukarejea kilingeni . Mungu wa Kabili akaniambia nipumzike, ikifika saa kumi na moja alfajiri niamke kwa ajili ya kupikwa. Akasema zoezi la kwanza lilikuwa kunisafisha na kuniosha kwanza, ambalo limeshakamilika, kinacho fuatia ni kupikwa.
NAPIKWA KICHAWI…
Ilipofika alfajiri nilidamka, kama nilivyo agizwa na mganga kwa ajili ya zoezi la kupikwa kichawi.. Nikaelekezwa kuingia katika chumba maalumu ambako kulikuwa na chungu kikubwa. Ndani ya chungu hicho yaliwekwa maji ya baharini, majani ya mti unaitwa muosha fedha ama mfedha mfedha, majani ya mkaratusi pamoja na majani ya mti unaitwa mkuyu, halafu ndani yake zikawekwa sarafu zilizoisha kutumika muda wake, pamoja na dawa nyingine kama tano hivi ambazo sikuambiwa ni dawa gani…
Baada ya hapo, nikaambiwa nikatwe nywele zangu, pamoja na kucha zangu. Baada ya kukatwa nywele zangu, vitu vyote hivyo vikachukuliwa vikafungwa kwenye kitambaa chekundu, ndani ya kitambaa hicho zikaongezwa dawa nyingine , halafu vikawekwa kwenye chungu kwa ajili ya kupikwa.
Katika chungu hicho pia vikawekwa visu saba, vikiwa vimesimama. Baada ya kama dakika kumi na tano hivi, mganga akamwambia msaidizi wake, ‘ hebu ongeza chumvi humo ‘. Nikatarajia kuona itakuwa chumvi ya kawaida ninayo ijua mimi, ila nikashangaa kuona kinawekwa kipande cha mti..
Baadae nilikuja kugundua kuwa, katika uganga na uchawi kuna kitu kinaitwa ‘Chumvi ya Kichawi” kazi ya chumvi ya kichawi ni kuukoleza uchawi ama kukoleza nguvu ya dawa.
Mganga aliniambia vitu vyangu yaani nywele pamoja na kucha vinaniwakilisha mimi, kwa hiyo kupikwa kwa vitu vyangu kunamaanisha mimi ndio nimepikwa. Baada ya dawa kupikwa, nikapewa maji yale na kuelekezwa kwenda kuoga. Nikaambiwa nikimaliza kuoga niende nikapumzike kwenye chumba change hadi nitakapo pewa maelekezo mengine.
NAFANYIWA TAMBIKO LA JUA .
Ilipo fika saa sita mchana, nikapewa dawa Fulani ya kujipaka, halafu nikapelekwa kwenye eneo la juani, ambalo chini kuna mchanga. Hairuhusiwi kuwa katika eneo hilo ukiwa na viatu. Baada ya kukaa katika eneo hilo kwa kama dakika arobaini hivi , mganga alianza kufanya uganga wake pale huku akitamka maneno yake ya kiganga. Baada ya hapo, akanifuata akanikabidhi kibuyu mkononi na kuniambia nikishike kwa mikono yangu yote miwili kisha nizungumz nizungumze maneno yafuatayo :
“ EWE JUA! MIMI NA WEWE, TU KITU KIMOJA SASA! WEWE NI MIMI NA MIMI NI WEWE. HAKUNA MTU YOYOTE YULE AWEZAE KUTUTENGANISHA.
EWE JUA!TANGU UANZE KUWEPO, HAUJAWAHI KUISHIA NJIANI.
VIVYO HIVYO, MIMI PIA, SITO ISHIA NJIANI. NITAFANYA MAMBO YANGU YOTE, NITAISHI MIAKA YANGU YOTE KWA KADRI MWENYEZI MUNGU ALIVYO NIKADIRIA , WALA HAKUNA MTU YOYOTE YULE ATAKAE WEZA KUNIZUIA, KWA CHOCHOTE KILE NITAKACHO TAKA KUKIFANYA…
KAMA WEWE JUA UMEWAHI KUISHIA NJIANI, BASI MIMI PIA, NITAISHIA NJIANI. NA KAMA KUNA MTU ANAWEZA KUKUZUIA WEWE JUA, BASI MIMI PIA NAWEZA KUZUILIKA. LAKINI KWA KUWA WEWE JUA HAUJAWAHI KUISHIA NJIANI, MIMI PIA, SINTOISHIA NJIANI. NA KWA KUWA HAKUNA MTU YOYOTE ANAYE WEZA KUKUZUIA WEWE JUA, BASI MIMI PIA, HAKUNA MTU YOYOTE ATAKAE WEZA KUNIZUA…
Niliagizwa kutamka maneno haya mara arobaini. Kila nilipo maliza kutamka, nilinyweshwa dawa na mganga, kutoka kwenye kibuyu alicho kuwa nacho…
Baada ya zoezi hili kukamilika tulirejea kilingeni ili lianze zoezi la ‘ kumtengeneza’ K, mume wa mtu mwenye pesa.
NAPEWA DAWA ZA KUMTEGA “K”
Tulipo rudi kilingeni, Mungu wa Kabili akaniambia nimpe majina yangu kamili pamoja na jina la huyo mwanaume ninae mtaka. Nikafanya kama alivyo niambia. Akayachukua yale majina, akaandika andika vitu vyake ambavyo sikuvijua vizuri, baada ya hapo akachukua kioo chake, akawa anatazama kwenye hicho kioo, kisha akachukua dawa kutoka kwenye kibuyu, akaweka kwenye chungu ambacho ndani yake kulikuwa na maji…. Baada ya kama dakika kumi na tano hivi, akaniangalia halafu akacheka sana.. Akaniambia niweke kiganja changu kwenye kile chungu nikafanya hivyo..
Basi akachukua dawa kutoka kwenye vibuyu vitatu, ambazo alizifunga kwenye vitambaa vitatu tofauti kila kitambaa na dawa yake, kisha akanipa dawa hizo na kunipa maelekezo yafuatayo : Dawa ya kwanza, utakunywa na maji ya kawaida, dawa ya pili, utaifunga kwenye mto unao lalia, halafu dawa ya tatu utaiweka chini ya kitanda chako.
Ndani ya siku mbili hizi, kuna kitu utakiona ukiwa umelala usiku. Kitakujia katika ndoto. Kitu hicho kina uhusiano na mwanaume unaye mtaka. Uki kiona kitu hicho tu, basi haraka sana nipigie simu nikuelekeze kitu cha kufanya.. Nikazichukua hizo dawa na kufanya kama nilivyo elekezwa.
NAMUONA “ K” KWENYE NDOTO.
Siku ya kwanza sikuona chochote, ila usiku wa siku ya pili, nikiwa nimelala usiku, niliijiwa na ndoto ya ajabu . Katika ndoto hiyo, nilimuona K akiwa anatembea kuja mahali kilipo kibanda changu cha genge.
Alipofika kwenye kibanda changu alisimama na kuniulizia kama nina hiriki. Kabla sijamjibu, ndoto ikakatika ghafla… Nilipo stuka na kutazama saa ilikuwa majira ya saa sita na ushee usiku.
Hapo hapo nikampigia simu Mungu wa Kabili na kumueleza nilicho kiona ndotoni… Akaniambia vizuri sana, kisha akaniuliza, je hilo eneo ambalo umemuona huyo mwanaume akiwa anatembea, unalifahamu. Nikamjibu ndio nalifahamu. Akaniambia, kesho saa kumi na mbili alfajiri, nenda kamwagie ile dawa niliyo kwambia uitunze chini ya kitanda. Baada ya hapo akaninisisitizia, “ Ukiisha fanya nae mapenzi, uje unione haraka iwezekanavyo, tufanye dawa za kumfunga..
Nikafanya kama alivyo nielekeza, alfajiri ya saa kumi na mbili, nikadamkia katika eneo hilo, kisha nikamwaga ile dawa halafu baada ya hapo nikarudi zangu nyumbani kujiandaa na kufungua genge langu.
NAINGIA KATIKA UHUSIANO WA KIMAPENZI NA “K” MUME WA MTU.
Saa mbili asubuhi nilifungua genge langu, nakumbuka siku hiyo ilikuwa Jumamosi. Mida ya kama saa nne hivi, K alikuja hadi gengeni kwangu na kununua vitu mbalimbali vya genge, kama vile karoti, nazi,pilipili manga nakadhalika na kurudi kwake.
Baada ya kama masaa mawili hivi, K alirejea tena pale gengeni kwangu, na kuchukua vitu vingine zaidi, halafu akaomba namba yangu ya simu, aka save namba yangu na mimi nikachukua yake, kisha akaondoka zake.
Baada ya kama nusu saa hivi, K akaanza kunitumia meseji za kunisifu. Alianza kwa kuniambia mimi ni mwanamke mchapakazi, najituma sana , nna hasira na maisha , nnafaa kuwa mama kwa sababu hata mume akifa anakuwa na uhakika watoto wake anawaacha na mwanaume imara.. Mwisho wa siku akanitongoza, na mimi sikulazia damu. Kesho yake, mimi na K tukakutana kimwili kwenye hoteli moja iliyopo maeneo ya Mbezi Beach.
Siku hiyo K akaniambia niachane na kazi ninayo ifanya, atanitafutia biashara nzuri ya kufanya, pia nihame pale nilipo kuwa nakaa, atanipangia nyumba inayo endana na hadhi yake.
NAPEWA DAWA ZA KUMPUMBAZA MUME WA MTU.
Mungu wa Kabili aliniambia, nikisha fanya mapenzi na huyo mwanaume, niende kwake ili anipe dawa za kumpumbaza. Nilipofika akaniambia, vitu vinavyo hitajika katika kutengeneza hiyo dawa ya kumpumbaza huyo mwanaume, ni NYWELE ZA MWANAUME MWENDAWAZIMU, NYWELE ZA MWANAUME ASIYE SIKIA ( KIZIWI ) , NYWELE ZA MWANAUME KIPOFU AU FIMBO ILIYO TUMIWA NA MWANAUME KIPOFU, KAMBA ILIYO TUMIKA KUMFUNGA KONDOO , pamoja na UCHAFU WA JALALANI.
Vitu vyote hivyo vilitafutwa vikapatikana, vikachanganywa na dawa nyingine za kichawi,kisha vikatumika kutengeneza uchawi. Nikaambiwa nitamuwekea kwenye maji ya kuoga na nyingine nitamuwekea kwenye chakula .
Halafu nikapewa na kibuyu, ndani ya kibuyu kile kulikuwa na kipande cha nyama. Mganga akaniambia hiyo ni nyama ya ndege wa usiku mwana wa jinni, ambayo baadae nilikuja kujua kuwa ni Bundi wa Kichawi, ambae ni tofauti na bundi wa kawaida.
Mganga akaniambia utapika nyama, katika nyama utakayo pika ambayo utamuwekea ndumba, mwanaume wako, utachanganya na nyama hiyo, pamoja na kucha zako, na nywele zako za siri.
Nilipo rudi nyumbani, nikafanya kama nilivyo elekezwa.
Baada ya kufanya uchawi huu, K alikuwa kama mwendawazimu kwangu, hakusikia wala kuambiwa na mtu yoyote Yule. Akawa anafanya kila ninacho taka akifanye mimi. Akaanza kuwa ananipa mali zake, magari, viwanja, nyumba, biashara pamoja na miradi yake..
NATEGA UCHAWI WA KUTOA MIMBA YA MKE MWENZANGU.
Mapenzi yangu na K yalipamba moto, nyumba aliyo nipangishia haikuwa mbali sana na mahali alipokuwa anaishi yeye na mkewe, wao walikuwa wanaishi Tabata Mawenzi, mimi akanipangia nyumba nzima Tabata Kimanga.
K alihama kwa mke wake, akawa anaishi nyumbani kwangu. Taarifa za K kuishi na “mchepuko” zilimfikia mke wake, lakini hakuwa na kitu cha kufanya kwa sababu K alikuwa ndio anamuweka mjini yeye na familia yake na mwanamke alikuwa mama wa nyumbani tu.
Mara nyingi K alikuwa ananishauri amfukuze mke wake, ili nikaishi nae kwenye nyumba yake, ili kuninonyesha kuwa ananipenda sana na mimi ndio kila kitu kwake.
Ila kuna kitu kimoja, alinifundisha Mungu wa Kabili, kwamba unapokuwa mchawi, unatakiwa uwe mnafiki. Usiache kabisa watu wajue kwamba una jambo Fulani kwa sababu ya uchawi . Hivyo nikawa najifanya kama namuonea huruma mke wa K lakini moyoni nilikuwa nataka afukuzwe mimi nikakae, pale.
Kuna kitu kimoja kilikuwa kinaniumiza moyo. Mke wa K alikuwa na ujauzito wa kama miezi mitano hivi. Sikutaka mwanamke huyo azae na K kwa sababu nilijua, angezaa na K mtoto angekuwa kiunganishi kwao, Mimi nilitaka K akisha achana na mke wake, basi iwe ndio moja kwa moja na kusiwe na chochote cha kuwaunganisha. Hivyo nikaanza kupanga njama za kuharibu ujauzito wa mke wa K kwa kutumia uchawi.
Suala hili nikalifikisha kwa Mungu Wa Kabili. Mungu wa Kabili akaniambia nitakupa dawa utaenda kutega kwenye mlango wake. Mti huo ni wa ajabu sana. Jina lake linafanana na jina la moja kati ya wilaya zilizopo kusini mwa Tanzania bara.
Baada ya kupewa dawa hiyo, nikafanya ujanja nikaenda kuitega kwenye mlango anaoutumia kupita. Alipo ruka mimba ikatoka. Kutoka kwa mimba ya mke wa K kulinipa sababu ya kurudi kwa mganga kwa ajili ya kuwatenganisha kabisa K na mke wake. Nilijua, majirani wangesema K kamuacha mke wake kwa sababu mke ana matatizo ya uzazi.
NAMTENGANISHA K NA MKE WAKE.
Nikarudi kwa mganga ili tufanye uchawi wa kumtenganisha K na mke wake. Mganga alichukua nyoya la ndege ambaye simfahamu jina lake, pamoja na dawa ambazo sikuzijua pia, akachukua majina ya K na mke wake, akaenda kuchoma jalalani.
Alipomaliza hapo, tukaenda kaburini, kwa ajili ya kuuzika rasmi uhusiano wa K na mke wake. Baada ya kuzika uhusiano wa K na mkewe, yalifanyika matanga kwa ajili ya kuomboleza “kifo’ cha ndoa ya K. Mganga alisema, kitu kilicho kufa, kinastahili kupewa maziko ya heshima. Usipofanya hivyo, roho ya kitu hicho itakusumbueni.
Niliporudi mjini nikakuta mke wa K kaondoka kwake, kahamia kwa dada yake. Mimi nikahamia moja kwa moja kwa K nyumba niliyokuwa nimepangiwa Kimanga nikamuweka mdogo wangu wa kiume.
NAANZA KUFUATILIWA NA NDUGU WA MKE WA ‘K’.
Ndugu wa mke wa K hawakufurahishwa na kuachana kwa K na mkewe, hivyo wakafanya kila juhudi kuwapatanisha, lakini msimamo wa K ulikuwa ni ule ule, kwamba hataki tena kuwa na mke wake na ameamua kuishi na mwanamke mwingine ambae ni mimi. K alikataa hata kushiriki kwenye vikao vya usuluhishi. Ndugu wote wa upande wake na upande wa mke wake wakawa wamemsusia K.
Watu wawili hawakutaka kukubaliana na matokeo. Nao ni baba wa mke wa K, pamoja na kaka mkubwa wa mke wa K. Watu hawa waligundua kilichotokea kati ya K na mke wake sio hali ya kawaida bali ni nguvu za ushirikina. Hivyo wakaamua kutafuta suluhisho kwa waganga. Walipo zunguka kwa waganga, hawakufanikiwa, hadi wakakata tamaa kunidhuru kwa njia ya uchawi.
Mwisho wa siku wakaamua, kunikodia majambazi, waje wanipige risasi. Walijua mimi ndio kikwazo kwa mtoto wao kurudiana na mume wake, hivyo njia pekee ikawa ni kifo tu.
Nilisurika kuuwawa na majambazi zaidi ya mara saba. Wakati huo Mungu wa Kabili alikuwa Lubumbashi nchini Kongo kwa shughuli zake. Alipo rejea nikamfuata kwa ajili ya kuomba ulinzi wake.
Kuna mnyama mmoja wa mwituni, ana ndimi mbili, yani ulimi wake una ndimi mbili, Mungu wa Kabili akatafuta ulimi wa mnyama huyo, mavi ya chatu pamoja na dawa zingine anazo zijua, lengo lake likiwa ni kuwatenganisha na kuwafarakanisha baba na kaka wa mke wa K ili wasipate nafasi ya kukaa pamoja na kunifuatilia.
Halafu baada ya hapo, akaagiza nipeleke mchanga wa kwenye kaburi la mtu aliyepita duniani bila kuonekana, ili anitengenezee dawa ya kuwafunga adui zangu wasinione. Pamoja na hivyo, akanipa hirizi iliyo tengenezwa kwa Mti Mkuu wa Wachawi.
Katika ulimwengu wa wachawi, mtoto aliye kufa akiwa tumboni kwa mama ake. Huitwa mtu aliyepita duniani bila kuonekana.
Nilivyo mpelekea udongo wa kwenye kaburi la mtu aliye pita duniani bila kuonekana, mganga akauchukua akafanya ulozi wake, halafu tukaenda wote hadi mtoni, akaenda akatega ndumba zake, pale, kesho yake tukakuta chura amenasa pale.
Wachawi wana amini, roho za watoto wanao kufa kabla hawajazaliwa, huwa zinaenda kuishi mtoni kama Chura. Lakini sio chura wote wapo hivyo, ni baadhi. Waganga wana utaalamu wao wa kujua chura yupi anahusika hapo.
Basi kaka na baba wa mke wa K, walikosana kwa ugomvi mkubwa, kiasi mtoto akawa anamtukana baba ake mzazi tusi la mama. Na kuhusu vitisho vya majambazi havikutokea tena
NATUMIA UCHAWI KUOKOA UHUSIANO WA KAKA ANGU.
Kaka angu ambaye nimempita miaka mitano, alikuwa anaishi kwenye nyumba ambayo K alinipangia. Nyumba hii ilikuwa maeneo ya Tabata Kimanga. Kaka angu alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke ambaye alikuwa Baa Medi kwenye bar inaitwa Mawenzi Garden.
Alimuachisha kazi ya ubaa medi baada ya mimi kumuwezesha kiuchumi kutokana na hela na mali nilizo hongwa na K pamoja na kumpa mradi mmoja wa K ausimamie. Mdogo wangu alimpenda sana mwanamke huyo .
Ila tatizo moja la mwanamke huyo, alikuwa na tabia ya umalaya. Umalaya ulikuwa kwenye damu yake .
Basi siku moja mdogo wangu alikuja kwangu kunishitakia kuhusu tabia ya wifi yangu. Mdogo wangu alikuwa anampenda sana mwanamke huyo, na alikuwa hawezi kumuacha kwa sababu yoyote ile, ila alikuwa anamuumiza sana kwa sababu ya tabia yake ya umalaya.
“ Ninampa kila kitu huyu mwanamke, ninampa hela, nimemfungulia biashara, nimempa gari, nawasomesha wazazi wake na kusaidia familia yake,. Lakini haridhiki tu, mwisho wa siku anatumia hela ninazo mpa kuhonga wanaume wengine.. ( HELA , GARI NA VITU VYOT AMBAVYO MDOGO WANGU ALIKUWA AKIMPA WIFI YANGU, VILIKUWA MALI YA K ALIZO CHUMA KWA JASHO LAKE NA MKE WAKE)
Nilimuonea huruma sana mdogo wangu, na nikaamini sio akili yake ila atakuwa amerogwa na mwanamke Yule. ( UNAJUA UKIWA MSHIRIKINA, KILA KITU UNAKUWA UNAAMINI KIMESABABISHWA NA USHIRIKINA )
Nikamwambia mdogo wangu usijali, kesho nitakwenda Bagamoyo kwa mtaalamu wangu, nitamuelezea tatizo lako, halafu nitamsikia atakacho niambia, nitakujulisha, ila usijali kama mwanamke huyo amekufanyia mambo ya Kiswahili, itajulikana tu na utakuwa huru.
Nilipo fika kwa Mungu wa Kabili, nikamueleza kila kitu, akaniomba majina ya mdogo wangu pamoja na jina la huyo wifi yangu, akatazama kwenye radar zake, halafu akacheka sana.
Mungu wa Kabili akaniambia, hakuna haja ya kumfunga mwanamke huyu. Huyu mwanamke ana sumbuliwa na damu ya umalaya. Umalaya upo kwenye damu yake. Hata tukimfunga kwa mdogo wako, tutakuwa tunajisumbua tu, atampenda sana mdogo wako, lakini atatoka nje tu kwa wanaume wengine. Hapa cha msingi, afanyiwe dawa ya kumfanya aache umalaya.
Mungu wa Kabili akachukua dawa moja inaitwa GEGEZI. Hii Gegezi ina ukubwa kama tunda linaitwa DADANSI na ina mibamiba.
Halafu akachukua dawa nyingine ambayo ni chakula cha ndege mmoja wa porini. Ndege huyo simkumbuki jina lake, ila ni mweusi, ana mdomo mrefu, ndege huyu akilia, vinyonga wote waliopo katika eneo hilo wanakimbia, huwa anakula vinyonga pia.,
Sasa ndege huyu huwa anakula majani ya mti Fulani wa porini ambao nimeusahau jina lake, hayo majani ndio ambayo Mungu wa Kabili aliya chukua.
Kitu kingine akachukua majani Fulani hivi, hayo majani ndio majani pekee yanayo liwa na mnyama wa porini ambae chakula chake kikuu ni nyama.
Pamoja na dawa hizo akachanganya na dawa zake nyingine ambazo sikuweza kujua ni dawa gani, halafu akaagizwa itafutwe minyoo ipatayo saba. Vito vyote hivyo vikaunguzwa pamoja kwenye chungu, hadi vikawa unga unga halafu vikachanganywa na mafuta ambayo sikujua ni mafuta ya kitu gani.
Mungu wa Kabili akanipa dawa hiyo akaniambia mpelekee kaka ako. Mwambie akiwa anafanya mapenzi na huyo mwanamke wake, afanye ujanja wake, achovye kidole chake kwenye hiyo dawa halafu akichomeke kwenye uke wa mwanamke huyo.
Tangu siku hiyo, mwanamke huyo hatokuwa Malaya tena . Nikafanya kama alivyo nielekeza na tangu mdogo wangu afanye hivyo, sikuwahi kumsikia tena akinipa kesi za wifi yangu, zaidi ya kumsifia mpenzi wake ametulia. Mwisho wa siku walifunga ndoa na kuzaa watoto.
NAMTEKA KICHAWI KIJANA WA KIARABU.
Nilimroga K kwa sababu ya pesa zake. Nikiwa kama mwanamke kamili, nilihitaji kuwa na mwanaume ninaye mpenda kutoka moyoni mwangu. Nataka nitoe funzo moja kwa wanaume, mnajua kila mwanamke alie olewa ambae hajaokoka huwa ana wanaume wawili. Mwanaume wa kwanza ni mwanaume ambae yupo nae katika ndoa, na mwanaume wa pili ni mwanaume ambae alitamani awe nae katika ndoa. Hivyo ndivyo ilivyo kuwa kwangu.
Sasa basi, kuna kijana mmoja wa kiarabu ambae nilikuwa namzidi umri kwa miaka minane. Kijana huyu aliishi mtaa wa pili kutoka nyumba niliyo kuwa nikiishi na K.
Nilitokea kumpenda sana kijana huyo lakini sikuwa na namna ya kumuanza, mnajua mwanamke kumtongoza mwanaume sio kazi rahisi. Nikaona isiwe tabu nikaamua kwenda kwa Mungu wa Kabili, ili anipe ndumba za kumnasa kijana huyo ambae kwa jina aliitwa Feisal.
Nilipo fika kwa Mungu wa Kabili akaniambia “ Inaonekana wewe ni mtundu mtundu sana,. Halafu naona una mambo mengi. Sasa nitakutengenezea uchawi, ambao utakuwa unautumia mwenyewe kumnasa mwanaume yoyote unae mtaka. “. Mungu wa Kabili akaniambia, njia hiyo itakuwa bora kuliko mimi kuwa naenda kumuona kila mara kwa jambo lile lile.
Mungu wa Kabili akaniambia, nitafute kopo linalo tumika chooni, nitafute nguo za marehemu. Hapa simaanishi nguo za maiti, la hasha nina maanisha nguo za marehemu.
Mfano wake ni kwenu kuna mtu amefariki, nguo zake zimegawiwa kwa ndugu, jamaa na marafiki, sasa nguo hizo ndio anazo zitaka.
Mungu wa Kabili, akaniambia niwe na uhakika kwamba nguo nilizo pewa ni nguo za marehemu kweli, hilo la kwanza, lakini pili niwe na uhakika kwamba marehemu huyo alikufa kifo cha Mungu na sio kachukuliwa msukule.
Nikamuuliza nitajuaje kuhusu mambo hayo, akaniambia ni rahisi sana. Wewe ukizipata nguo za marehemu, au mtu atakae kuuzia nguo za marehemu, basi akuonyeshe mahali lilipo kaburi la marehemu, halafu utakuja kwangu nikuelekeze cha kufanya.
( KATIKA ULIMWENGU WA WACHAWI, NGUO ZA MAREHEMU NI BIASHARA KUBWA SANA, KUNA WATU WANAISHI KWA KUFANYA BIASHARA YA KUUZA NGUO ZA MAREHEMU MBALIMBALI..MIMI MWENYEWE NILIUZIWA NGUO ZA MAREHEMU KWA BEI MBAYA ).
Baada ya kufanikiwa kupata nguo za marehemu, pamoja na kuonyeshwa mahali lilipo kaburi la huyo marehemu, nilirejea kwa Mungu wa Kabili.
Mungu wa Kabili alizichukua zile nguo, akakata kipande kidogo kwenye shati moja, akapaka mafuta ambayo sikujua ni mafuta ya nini, akazifunga kwenye kitambaa chekundu, akaweza kwenye kibuyu, ndani ya kibuyu hicho akaweka yai la kuku mweusi, sindano saba pamoja na mafuta mengine ambayo sikujua ni mafuta ya nini ila wao wachawi na waganga wanayaita mafuta ya usiku, kisha akakifunga kile kibuyu, halafu akanikabidhi, akaniambia, ikifika usiku wa saa moja , nenda hadi kwenye hilo kaburi, kisha ukiweke kibuyu hicho juu ya hilo kaburi kwa kukilaza., halafu asubuhi pita katika kaburi hilo uangalie kwa makini kibuyu hicho, ukikikuta bado kimelala kama ulivyo kiacha basi ujue huyo marehemu kweli amekufa kifo cha Mungu, lakini ukikuta kimesimama, basi marehemu huyo bado yupo hapa hapa duniani, amechukuliwa msukule.
Nikafanya kama alivyo niagiza, na kweli kesho yake nikakuta kibuyu kimelala kama nilivyo kiweka. Mungu wa Kabili akaniambia nguo hizo zinafaa kwa ajili ya kutengeneza dawa hiyo.
Basi akachukua hizo nguo, akaziunguza kwenye chungu cheusi pamoja na dawa nyingine kama aina kumi na mbili, halafu akazihifadhi kwenye kibuyu na kunikabidhi, pamoja dawa zingine kwenye vifuko vitatu.
Akaniambia, ukimtaka mwanaume yoyote Yule, utamuita kwa kutumia dawa hii… Mwanaume utakae muita sauti yako ataisikia na kuitii mara moja kama ambavyo marehemu huyo alivyoitwa na Mungu na kuitii sauti yake.
Mungu wa Kabili akaniambia huo ni uchawi mkubwa sana katika mapenzi, hakuna mwanaume nitakae muita na akakataa kuitika. Uchawi huu hautumiki katika mapenzi tu, hata kama mambo mengine, ilimradi unacho taka wewe ni kumuita mtu.
Kitu kingine akaniambia, ukimuita mwanaume kwa kutumia uchawi huu zaidi ya mara saba, halafu akakataa kuitika, basi jua kwamba mwanaume huyo kinga yake ni kubwa sana.
Sasa basi ukisha ligundua hilo, unatakiwa kutuma nyoka wa kichawi kuua kinga ya mwanaume huyo. Ukisha ua hiyo kinga, muite tena mwanaume huyo na atakuja haraka sana.
Nyoka huyu sio nyoka wa kawaida kama nyoka wengine. Ni nyoka wa kichawi. Ni jinni. Mungu wa Kabili akanikalisha kwenye kigoda na kuniambia, “ Nitamtengeneza nyoka huyu, halafu nitakukabidhi, umtunze vizuri kwa kufuata masharti yake…”
Katika kumtengeneza nyoka wa kichawi, Mungu wa Kabili akachukua kitovu cha mtoto. ( KUWENI MAKINI SANA NA MAHALI MNAPOVITUPA VITOVU VYA WATOTO WENU.. KATIKA ULIMWENGU WA WACHAWI VITUVO VYA WATOTO NI BIASHARA KUBWA SANA… KITOVU CHA MTOTO KINAPOENDA KUTUPWA, AMA KUFUKIWA, KATIKA WATU WANAO PEWA JUKUMU LA KUVITUPA, HUWA KUNA MMOJA WAPO ANAWEZA KUWA SIO MUAMINIFU, HUENDA KUFUKUA MAHALI KILIPOFUKIWA NA KWENDA KUKIUZA KWA WACHAWI NA WAGANGA )
Alipochukua hicho kitovu, akakifunga kwenye mti wa mnyonyo, halafu akanyunyizia dawa kutoka kwenye vichupa kama saba. Baada ya hapo akachukua uzi mwekundu, akafunga vifundo saba kwenye kamba hiyo, halafu akatupa kwenda chini, ilipotua tu, ikageuka kuwa nyoka. Akamshika huyo nyoka, akamuhifadhi kwenye kibuyu cheusi, chenye shanga juu, akafunga na kitambaa cheusi na kunikabidhi.. Akanielekeza jinsi ya kumtuma nyoka huyo kufanya kazi mbalimbali pamoja na masharti yake.
Kuhusu lile kopo la chooni, Mungu wa Kabili akaniambia amelitumia kutengeneza dawa ya kujua siri za watu. Dawa hiyo itanisaidia kujua kama mwanaume niliye nae ana hela au hana hela, ana mke au hana mke. Ana watoto au hana watoto.
Kingine akanikabidhi ua ambalo natakiwa kulipanda nyumbani. Kupitia ua hilo nitakuwa ninajua kama mwanaume ambae nipo nae amepata hela au la.
Kitu cha mwisho, akaniambia, kwa sababu nnaonekana nnapenda sana wanaume, inabidi anipe dawa ya kuwatengeneza wanaume nitakao kuwa nao na kuwafanya kutokuwa na uwezo wa kufanya mapenzi na wanawake wengine isipokuwa mimi tu. Hii itasaidia kuniepusha na magonjwa kama vile ukimwi nakadhalika.
Mungu wa Kabili akanipa mti mmoja mrefu, akaniambia katika mti huo, utatumia zaafarani nyekundu au ya njano, kuandika majina ya wanaume wote ambao upo nao kimapenzi pamoja na jina lako, ukisfanya hivyo, nenda kautegeshee barabarani, ukishagongwa na gari tu, basi wanaume hao watakuwa wakikutana na wanawake wengine, uume wao unakuwa haufanyi kazi.
Nilivyo rudi nyumbani nikafanya kama nilivyo elekezwa na kweli Yule kijana alikuja mara moja tangu nilipo muita. Nilifurahi sana kumpata Feisal. Pamoja na kwamba nilikuwa nimemuita kichawi ila nilikuwa namuheshimu sana kwa sababu nilikuwa nampenda toka moyoni mwangu.
Baada ya kama wiki mbili tangu nianzee uhusiano wangu na Feisal, nikagundua Feisal ana tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume. Uwezo wake kitandani ulikuwa mdogo sana.
Kama kawaida yangu nikaenda kumuona Mungu wa Kabili. Mungu wa Kabili akanipa dawa moja inaitwa KISHINDO. Akaniambia utakuwa unachemsha unampa anakunywa glasi moja asubuhi na nyingine anakunywa jioni, kwa siku kumi mfululizo. Nikafanya kama alivyo nielekeza. Baada ya kumpa Feisal dawa hiyo, nilijilaumu kwanini nilifanya hivyo. Uwezo wake kitandani ulikuwa wa ajabu, alikuwa anashiriki tendo kwa muda mrefu sana na alikuwa akirudia mara nyingi bila kuchoka…
NAMFANYIA VITUKO K
Katika muda wote huo, nilikuwa bado ninaishi na K kwenye nyumba yake ya Tabata Mawenzi. K alikuwa kama Ndondocha kwangu. Kwanza nilikuwa simpi unyumba na nilikuwa nafanya kila kitu ninacho taka kukifanya tena mbele yake.
Feisal alikuwa anakuja nalala nae chumbani, K analala pepe yake kwenye chumba kingine. Alikuwa anafanya kazi zote kama vile kufua, kufanya usafi na kila aina ya kazi ambayo houseboy anatakiwa kuifanya.
Na katika kipindi hiki K alikuwa ameshafukuzwa kazi kutokana na uzembe kazini. Mimi mwenyewe nilimpiga marufuku kwenda kazini kwa mwezi mmoja, nilimwambia achague kitu kimoja kati ya kwenda kazini au kufanya kazi zangu.
Sasa basi nikawa namfanyia K vituko, lengo langu nikitaka aondoke mwenyewe aniachie nyumba na mali zake. Hakuwa na faida yoyote tena kwangu. Kazi ameshafukuzwa , mali zake zote pamoja na biashara zake ninazimiliki mimi.
Basi kila nilipokuwa nikifanya mapenzi na Feisal nikawa napiga kelele ili kumuudhi K. Na hivi Feisal alikuwa anatumia muda mrefu basi na kelele zangu zikawa za muda mrefu. Lakini wapi, K wala hata hakuonyesha dalili ya kwamba anaweza kuondoka , undondocha ulikuwa umetamalaki kwenye kichwa chake.
Kwa kutumia ndumba hizo nilizo pewa na Mungu Wa Kabili, niliwateka kichawi wanaume wengi na kuvunja ndoa nyingi sana.
K ANAAMUA KURUDI KIJIJINI
Nilipoona K hana dalili ya kuondoka pamoja na kumfanyia vituko lukuki, nikaona niende kwa Mungu wa Kabili ili kama kuna uwezekano wa kumfukuza K kichawi.
Nilipofika kwa Mungu wa Kabili, akafanya dawa zake, halafu ikatengenezwa ngalawa ndogo, nikaambiwa nipeleke nguo yoyote ya K . Nguo ya K ikafanyiwa uchawi halafu ikafungwa kwenye hiyo ngalawa, tukaenda baharini kutegea wakati bahari imesafiri tukaenda kuiweka ngalawa , maji yalipokuja yakaondoka na hiyo ngalawa, kesho yake tu, K mwenyewe akasema anataka kwenda kusalimia kijijini kwao amepakumbuka. Nilifurahi sana niliposikia hivyo, nikamfungia nguo zake, nikampa na nauli pamoja na hela ya kula njiani..
Kalivyo rudi kwao, baadhi ya ndugu zake hawakuridhishwa na hali ya K pamoja na maelezo yake. Mtu aliyekuwa tegemeo la ukoo mzima, ghafla anarudi kijijini akiwa hana kitu na maelezo yake yanatatanisha. Wakaamua kufunga safari hadi mjini ili kufuatilia mali za ndugu yao. Nilipo pata taarifa zao, nikaenda kuwashitaki kwa Mungu wa kabili, wote walipeperuka na sikusikia chochote kuhusu watu hao.
NAINGILIA NDOA YA WALOKOLE.
Nilitokea kumtamani mwanaume mmoja mlokole alieishi mtaa wa pili kutokea nilipokuwa naishi. Huyu nilimpenda kama nilivyo mpenda Feisal. Alikuwa mkaka mzuri anae jipenda sana. Kwa jina aliitwa Erasto. Kikwazo kikubwa kwa Erasto ilikuwa, kwanza alikuwa ameokoka na pili alikuwa na mke ambaye alikuwa ameokoka pia. Mke wa Erasto alikuwa na ujauzito mkubwa tu wa kama miezi mitano au sita .
Nasema kuokoka ilikuwa kikwazo kwa sababu Mungu wa Kabili Alisha nishauri niwe makini sana na walokole kwa sababu wana nguvu za ajabu. Ila akaniambia kuna walokole wa waina mbili., mlokole wa ukweli na mlokole feki. ..
Hivyo basi kama umemempenda mwanaume wa kilokole, unatakiwa kwanza umpime kichawi kujua kama ni mlokole wa ukweli ama mlokole feki.
Akaniambia uchawi unao tumika kupima nguvu ya mlokole, sio uchawi wa kitoto, hauwezi kufanywa na mtu yoyote, akaniambia kama itatokea nimempenda mwanaume wa kilokole, basi niende kwake halafu yeye atampima kama mlokole huyo ni orijino au feki.. Kama ni orijino una achana nae kwanza unatafuta njia nyingine ya kumpata, lakini kama ni feki,unamvuta kama watu wengine.
Akaniambia, ukimpenda mwanaume wa kilokole orijino ni bora utumie njia za kawaida kumteka, kuliko njia za kichawi, kwa sababu kwa njia za kawaida, ataishia kukukemea tu,. Lakini kwa njia ya uchawi, utapigwa shot. Hakuniambia ni shoti gani.
TUNATUMIA UCHAWI KUPIMA ULOKOLE WA ERASTO.
Ili kujua kama mlokole ni orijino au feki, wachawi hutumia nzi. Hivyo basi Mungu wa Kabili alianza kufanya uchawi ili kupima kama Erasto ana nguvu za Mungu au hana nguvu za Mungu.
Siku hiyo Mungu wa Kabili akachukua bakora ya kichawi ambayo imetengenezwa kwa mti wa Mkomoro, Mganga akaniambia mti huo wa mkomoro ni mti wenye nguvu nyingi sana za kichawi na wachawi huutumia kwa mambo mengi ikiwa ni pamoja na kufufua wafu.
Mungu wa Kabili akaanza kwa kuwaita inzi na kisha kuwatuma waende kwa Erasto ili kujua kama ana nguvu za Mungu au la. Lilikuja kundi la nzi wengi, na walipo tua tu kwenye fimbo yake wote wakapasuka pale pale.
Mungu wa Kabili akaniambia kwa kunisisitiza, achana kwanza na huyu Erasto, kesho ninasafiri kwenda Mkuranga , nitakuwa huko kwa siku saba tunaenda kupika uganga . Nitakapo rudi tutaangalia njia nyingine ya kumteka Erasto.
Waganga na wachawi huwa wanakuwaga na MWAKA WA UCHAWI ama MWAKA WA UGANGA, kama ambavyo kuna MWAKA WA FEDHA, MWAKA WA MASOMO nakadhalika.
Unapofika mwaka wa uganga, waganga hukutana mzimuni na kupika uchawi, ambao huuzwa kwa waganga mbalimbali. Jambo hilo hufanyika kila mwaka.
Mungu wa Kabili alikuwa anaelekea Mkuranga kwa ajili ya kusimamia zoezi la upikaji wa uchawi unaoitwa MANGUBE. Kwa hiyo Mungu wa Kabili akaniambia nisubiri kwanza mpaka wiki mbili zipite ndio tuje tukae tupange cha kufanya juu ya Erasto, kwa sababu baada ya kutoka Mkuranga alikuwa anaelekea Liwale Lindi.
Sikuwa na jinsi zaidi ya kukubaliana na maagizo ya Mungu wa Kabili.
NAMTUMIA ERASTO NYOKA WA KICHAWI.
Baada ya siku tatu uvumilivu ukanishinda, nikaamua liwalo na liwe, kama kuna baya litanitokea, Mungu wa Kabili atanisaidia.
Usiku wa saa sita siku hiyo, nikamchomea Erasto, dawa ya kumvuta kwangu kichawi. Kwa kawaida nikishachoma dawa, usiku huwa naota nafanya mapenzi na mwanaume nilie mchomea dawa na kesho yake, kabla ya saa sita mwanaume huyo huwa ananitafuta, lakini kwa Erasto ikawa tofauti. Sikuona chochote. Nikachoma kwa siku saba mfululizo hakuna chochote.
Nikakumbuka Mungu wa Kabili aliniambiaga kwamba, kama nikichoma dawa ya kumuita mtu na mtu huyo asije, basi nijue kuwa mtu huyo ana kinga kubwa, kwa hiyo natakiwa nimtumie nyoka wa kichawi, nyoka huyo ataenda kuvunja kinga ya mtu huyo.
Siku hiyo usiku wa saa sita, nikaenda kuchukua kile kibuyu ambacho kilitumika kumuhifadhi Yule nyoka, nikamtuma nyoka huyo aende kuigonga na kuivunja kinga ya Erasto. Nilipomaliza kunena maneno yangu nikafungua kile kibuyu ili nyoka atoke, nyoka alipotoka akanigonga kwenye mguu na kutokomea.
Nilipiga kelele za ajabu, house girl wangu akaenda kuwaamsha majirani na kupiga simu ya kaka angu, nikapelekwa hospitali, hospitali nikapimwa lakini hakikuonekana kitu, wala haikuonekana kama nina sumu yoyote mwilini, lakini nilikuwa nasikia maumivu makali sana yaliyokuwa yanakuja na kuondoka, nikapewa dawa za kuzuia maumivu lakini wapi. Ilipofika asubuhi maumivu yakawa yameisha lakini nikawa nimepooza upande mmoja.
Nikamwambia kaka angu apige simu ya Mungu wa Kabili, lakini Mungu wa Kabili alipopigiwa na kuelezewa kilicho tokea, akawa mkali sana, kwanza akasema alinionya nisifanye chochote halafu pili akasema hawezi kunisaidia kwa namna yoyote ile.
Sikuwa na jinsi zaidi ya kumueleza kaka angu ukweli. Kilicho fuatia tukaanza kuzunguka kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya tiba yangu lakini wapi. Baada ya wiki mbili nilipelekwa kwa Mungu wa Kabili Bagamoyo angalu aione hali yangu ilivyo labda anaweza kunionea huruma lakini, akakataa kata kata…. Msimamo wake ulikuwa ni ule ule, nimefanya jambo ambalo alinikataza kulifanya na pia hana uwezo wa kunisaidia. Zaidi aliniambia hatima yangu ni kifo.
Tulizunguka kwa waganga wa kila aina na kila sehemu lakini wapi hali yangu ikazidi kuwa mbaya.
Siku moja ndugu yangu mmoja wa upande wa mama angu, alikuja kuniona baada ya kusikia nimepooza. Baada ya kumsimulia kuhusu kisa changu alisikitika sana. Nikapelekwa kwenye kanisa moja la kiroho na kuombewa. Siku tatu tangu nianze kuombewa nilitapika vitu vingi sana vya ajabu ajabu, kama vile kucha, nywele, damu nakadhalika, na taratibu hali yangu ikaanza kutengemaa na hatimaye nikapona kabisa.
Namshukuru Mungu sasa hivi nimeokoka, nimempokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yangu. Mali za K nimezirudisha na sasa ninaishi maisha yangu halali kwenye chumba cha kupanga maeneo ya Mbezi Ya Kimara.
Ninaumia sana moyoni kuona, nimeseababisha mateso kwa wanawake wenzangu, nimevunja ndoa za watu. Nimeamua kumtumikia Mungu katika maisha yangu yote. Ninawaomba msamaha wale wote nilio waharibia maisha.
CHA MWISHO NA KIKUBWA.. NAWATAHADHARISHA WANAWAKE WENZANGU KUHUSU WAGANGA WA KIENYEJI
10 Sept 2017
New
mulo
Mahusiano