KUFUATIA Rais Dkt. John Magufuli kueleza jana Mjini Dodoma kuwa Serikali imebaini kwamba Kampuni ya Mawasiliano ya Airtel ni mali ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na kumwagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango kufuatilia suala hilo haraka ili Airtel irudishwe kumilikiwa na serikali, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL Omary Rashid Nundu ameamua kuweka wazi rafu zilizochezwa wakati wa ununuzi na umiliki wa hisa za Airtel.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Desemba 21, Nundu ameema wao kama TTCL hawamiliki chochote kwenye Kampuni ya Airtel.
“Wamiliki ni serikali yetu na ubia wa Bharti Airtel. Sisi kama TTCL tulianzisha Celtel mwaka 2001 na mtu asiyejulikana ambaye hisa yake ilishikiliwa na raia wa nje. Ilipofika Novemba 27, 2001 hisa ya mtu asiyejulikana ilishikwa na Mtanzania ambaye alikuwa kwenye Bodi ya TTCL pia kwenye Bodi ya Celtel.
“Agosti 5, 2005 ilikuwa ni siku ya vioja kwani aliyekabidhiwa hisa moja ya asiyejulikana ndiyo akawa mwenyekiti wa kikao cha bodi, alirudisha hisa kwa TTCL, bodi ikaongeza thamani ya kampuni na dola Mil. 40 alipewa kama mtaji wake.
“Agosti 5, 2005 kwenye Kikao cha Bodi ya TTCL ikawa mmiliki kwa asilimia 100 wa Celtel lakini cha kushangaza baada ya saa kadhaa, TTCL ikanyang’anywa hisa zote siku hiyohiyo, zikagawanywa kwa watu wengi. Hapo uhalali wa kunyang’anywa hisa zile ni upi? alihoji Nundu na kuongeza,
“Kilichotokea hisa za Celtel ziligawiwa kwa watu ambao hata hawakuwepo kwenye kuanzisha Celtel, pia uwiano wa hisa haukuwa sawa wala. Mbali na hilo kuna hisa ailizogawiwa mwekezaji na hazikumilikiwa, mwekezaji akawa na asilimia 60 na kuwa na share nyingi zaidi.
“Mtaji waliyolipa ni nusu ya thamani ya hisa zao lakini hakuna aliyewahi kukopeshwa hisa duniani. Tukiamua kukusanya hasara iliyopatikana ni kubwa. Utagundua Airtel ya leo ina historia ndefu na TTCL,” alieleza Nundu.
Aidha Waziri Kindamba Afisa Mtendaji Mkuu TTCL amesema alichosema Rais Magufuli jana ni “tip of an iceberg”, alichokonoa tu huku akisema wizi uliofanywa lazima uwekwe wazi. Ameeleza pia kuwa kuna mambo yalifanyika kwenye kampuni ya simu tangu kuanzishwa kwake dhidi ya TTCL ambapo Watanzania wameibiwa rasilimali zao.