Makamu wa Rais Zanzibar Afunguka Kuhusu Suala la Kuongeza Muda wa Urais - MULO ENTERTAINER

Latest

16 Dec 2017

Makamu wa Rais Zanzibar Afunguka Kuhusu Suala la Kuongeza Muda wa Urais

Makamu wa Rais Zanzibar Afunguka Kuhusu Suala la Kuongeza Muda wa Urais

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema ushauri wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutaka kuongezwa muda wa urais madarakani badala ya miaka mitano iwe miaka saba ni suala ambalo zuri na linazungumzika bila ya matatizo.


Balozi Iddi aliyasema hayo leo Ijumaa Desemba 15 wakati akifunga mkutano wa nane wa Baraza la Tisa la Wawakilishi lilichukua muda wa wiki moja Zanzibar.

Awali baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wakichangia Mswada wa Sheria ya Marekebisho ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 1984 na kuweka sheria ya mwaka 2017, walisema kuwa ili Zanzibar kuepukana na matumizi hasa kipindi cha uchaguzi hakuna budi kuongezwa kwa muda wa utumishi wa urais.

Mmoja wa  wawakilishi hao wa Jimbo la Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma amesema kuwa ili kumpa Rais wakati mzuri wa kutumikia wananchi ipasavyo hakuna budi muda wake kuongezwa zaidi ili kuona kuwa ile mipango ya kufikisha maendeleo kwa wananchi iweze kufanikiwa.

Amesema kwa kuwa muda wa miaka mitano wa uongozi wa Rais madarakani ni mdogo na kuonekana kupoteza fedha nyingi za wananchi kwa kufanya uchaguzi kila miaka mitano, ni vyema uongozi kuliona hilo na kulifanyia kazi.

Amesema kuwa kwa mujibu wa tathmini yake ya uchaguzi Mkuu mara nyingi hutumia fedha nyingi za walipakodi kiwango ambacho kinaweza hata kujenga zaidi ya shule kubwa 20 ambazo zingesaidia jamii katika kuondokana na uhaba wa shule.

Amesema kuwa pamoja na katiba zote mbili ya Tanzania bara na Zanzibar kuweka muda huo wa miaka mitano lakini bado kuna nafasi kubwa kwa Zanzibar kufanya marekebisho ya katiba yao ili kuongeza muda, akidai kuwa ni jambo ambalo haliwezi kuathiri hata kidogo katiba ya Tanzania.

Juma amesema pindi ikiamuliwa kufanyika hivyo ni wazi kuwa faida kubwa inaweza kupatikana ikiwamo Rais kupata muda mwingi wa kutumikia jamii badala ya muda wa sasa miaka mitatu tu ya kutumia jamii huku miaka miwili iliyosalia akishughulikia masuala ya uchaguzi.

Balozi Iddi akitolea ufafanuzi suala hilo amesema kwa kuwa jambo hilo linahusiana na pande mbili za Muungano ni vema kwa wakati huu suala hilo likaachiwa kwa viongozi husika kwa kulifayia kazi ikionekana linafaa ni wazi linaweza kupunguza gharama kubwa hasa kwa upande wa chaguzi za viongozi wakuu.

“Hili itakuwa si suala jipya kwetu kwani hata ndugu zetu wa Rwanda nao wameongeza muda wa uongozi, hivyo nasi tukibadili miaka badala ya mitano tukaweka saba tunaweza kufanikiwa kimaendeleo kwa hatua kubwa,” amesema Balozi Iddi.