Maalim Seif: CUF haitoshiriki uchaguzi wowote chini ya Tume ya Jecha Salim Jecha - MULO ENTERTAINER

Latest

23 Mar 2016

Maalim Seif: CUF haitoshiriki uchaguzi wowote chini ya Tume ya Jecha Salim Jecha

SIKU mbili tangu kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Zanzibar, na siku moja kabla ya kuapishwa Dk Ali Mohamed Shein, Maalim Seif Shariff Hamad, Mgombea wa Urais wa Zanzibar katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana kupitia Chama cha Wananchi (CUF), amesema CUF haitashiriki uchaguzi wowote chini ya Tume ya Jecha Salim Jecha.

Akizungumza na MwanaHALISI Online Hoteli ya Serena ambapo yupo kwa mapumziko baada ya kulazwa, Maalim Seif amesema kuwa kama yatatokea maridhiano yatakaoongozwa na kusimamiwa na taasisi huru za kidemokrasia, bila vitisho vya majeshi na polisi, kuwa na vyombo huru vya habari na tume huru sio hii iliyopo Zanzibar chini ya Jecha, hapo CUF kitaweza kufikiri kushiriki uchaguzi.

Ameongeza kuwa harakati za kudai haki, zitaendelea kwa njia ya amani ili marekebisho ya tume yafanyike kwani kwa utaratibu uliopo hata mwaka 2020 upinzani ukishinda Tanzania bara, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitang’gang’ania madaraka.

“CUF tunaamini katika amani, tusichafue amani, tusichafue nchi yetu, tuendeleze mapambano kwa kutoitambua serikali iliyojiweka madarakani katika uchaguzi haramu wa Machi 20 mwaka huu, wala hatutaipatia ushirikiano wowote katika mambo yote” alisema na kuongeza :

"Uchaguzi wa 20 Machi, sio halali. Jecha hakuwa na uwezo wa kisheria wala kikatiba kufuta uchaguzi, mgogoro uliopo sasa umesababishwa na Jecha, ukapewa baraka za CCM, sababu CCM hawataki kushindwa, na hawataki wapinzani kuongoza. Kila CCM ikishindwa hutoa visingizio.

“Kabla Kikwete (Rais Mstaafu Jakaya Kikwete) hajaondoka madarakani, aliniambia kuwa Maalim CCM wanakuogopa, wanajua ukishinda utaweza kuvunja Muungano, lakini nilimwambia, CCM ndio wenye jeshi, wenyewe ndio wenye dola mimi nitavunjaje Muungano?

"Hiyo ni hofu na visingizio tu ili waendelee kukwapua madaraka.”Alisema.

Ameweka bayana kuwa kwa sasa CCM imewarejesha wananchi miaka 20 iliyopita, kwani uhasama wa watu kutengana kwenye shughuli za kijamii kwa sababu za tofauti za kisiasa zimeanza kurejea baada ya CCM kulazimisha kukwapua madaraka ya wananchi kwa kufuta uchaguzi wa 25 Oktoba mwaka jana.

Akizungumzia suala la Muungano kama ambavyo amekuwa akihusishwa Maalim seif amesema kuwa sasa Muungano utavunjwa na CCM, sio CUF wala yeye kama wanavyosingizia.

Ameongeza kuwa kwa sababu CCM ya bara ndio inalazimisha kuweka viongozi waliokataliwa na wananchi wa Zanzibar na chama chao kwa kutumia majeshi na polisi wao ndio husababisha wananchi wachukie Muungano.

Aidha kuhusu uchaguzi wa marudio wa Machi 20, Seif amesema kuwa CUF imeshinda, kwani wananchi wa Zanzibar waliitikia wito wa CUF, wakasusa, hawakujitokeza kupiga kura.

“Mimi nilishasema tangu awali, kuwa matokeo yameshajulikana kabla ya uchaguzi, sababu ni ya kupika, namhurumia Dk Shein kwa kujisifu kupata kura ambazo hazipo, mawakala waliweka wao na wasimamizi na kuna taarifa kuwa wapigakura walikuwa wanapewa rundo la kura, wapige na kutumbukiza ili kukidhi matakwa ya CCM.” Amesema Maalim Seif.

Maalim Seif amewatakia utulivu Wazanzibar wote, na kuwaarifu kuwa afya yake ni imara, na atarejea Zanzibar wakati wowote kuungana nao.