Mwijage Afunguka Kuhusu Mgogoro wa Biashara na Kenya - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Sept 2018

Mwijage Afunguka Kuhusu Mgogoro wa Biashara na Kenya

Mwijage ajibu kuhusu mgogoro wa biashara na Kenya
Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema Tanzania haina mgogoro wa kibiashara na Kenya licha ya nchi hizo mbili kupitia mamlaka zake kuzuia bidhaa mbalimbali zinazoingizwa kwenye  nchi hizo.


Septemba 13 na 15 mwaka huu kulisambaa taarifa kuwa mamlaka ya mapato ya Kenya KRA ilizuia malori ya mchele yaliyotoka Tanzania kwa madai ya mchele huo kutokua na viwango vya ubora vilivyowekwa na nchi hiyo.

November 2017 kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi waliviteketeza kwa moto vifaranga vya kuku 6,400 na Februari 2018 viliteketezwa vifaranga 5000 kwa kuingizwa bila kufata taratibu na sheria za nchi.

Akizungumza East Africa Radio kupitia kipindi cha East Africa Breakfast Waziri Charles Mwijage amesema serikali ya Kenya na Tanzania hazina mgogoro wa kibiashara bali kinachofanyika ni usimamiaji wa taratibu zilizowekwa na mamlaka za nchi hizo  huku akiahidi kulifatilia suala la malori ya mchele ya Tanzania yaliyozuiliwa Kenya.

“Nimelisikia hilo suala la kuzuiwa kwa malori ya mchele ya Tanzania, kimsingi hatuna mgogoro wa kibiashara kati yetu na jirani zetu (Kenya) bali ninachowahasa wafanyabiashara wetu wazalishe vitu vyenye ubora unaoendana na viwango vya mataifa wanayopeleka bidhaa zao.”

Februari mwaka huu  nchini Uganda  Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta waliwaagiza mawaziri wa pande zote mbili zote kukutana kabla matatizo yanayojitokeza hayajifika kwenye ngazi yao.